SHAMBULIO LA ANGA LAUA NA KUJERUHI GAZA

Watu watatu wameuawa na wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la anga la Israel kwenye ghorofa moja mashariki mwa Jiji la Gaza.

Kwa mujibu wa mwandishi wetu, shambulio hilo lililenga ghorofa inayomilikiwa na familia ya Ahmad Hamada, karibu na Shule ya Yafa katika mtaa wa Al-Tuffah, mashariki mwa Gaza. Ahmad, mke wake, na mtoto wao waliuawa kwenye shambulio hilo.

Vilevile, vikosi vya kijeshi vya Israel vilifyatua risasi kwenye nyumba za raia mashariki mwa kambi ya wakimbizi ya Al-Bureij, katikati mwa Ukanda wa Gaza, na kusababisha majeraha kwa raia kadhaa. Walioumia walipelekwa Hospitali ya Mashahidi wa Al-Aqsa mjini Deir al-Balah.

Kwa upande mwingine, vikosi vya majini vya Israel vilishambulia eneo la karibu na Daraja la Wadi Gaza kaskazini magharibi mwa kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, huku ndege za kivita za Israel zikishambulia nyumba moja katika Barabara ya Salah al-Din, kwenye kiingilio cha kambi ya Nuseirat. Pia, mizinga ya Israel ilifyatua makombora kwenye mitaa ya Tel al-Hawa na Al-Zeitoun ndani ya Jiji la Gaza.

Ndege za kivita za Israel ziliendelea kushambulia maeneo ya Deir al-Balah katikati mwa Gaza, na sehemu za mashariki mwa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza. Mizinga ya Israel pia ilishambulia eneo karibu na Minara za Sheikh Zayed mashariki mwa Beit Lahia kaskazini mwa Gaza, na eneo la magharibi mwa Rafah kusini mwa Gaza.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilithibitisha katika ripoti yake ya jana kuwa mabomu na uhasama unaoendelea vimesababisha vifo, majeruhi, na kuwahamisha watu, huku vikiharibu miundombinu.

Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa iliripoti kwamba katika saa 48 zilizopita, shule tatu ambazo zilikuwa zinahifadhi wakimbizi huko Gaza zilishambuliwa, na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Post a Comment

0 Comments