WHO YALAANI VIKALI SHAMBULIO LA ISRAEL DHIDI YA HOSPITALI YA AL-AHLI ARAB KASKAZINI MWA UKANDA WA GAZA.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limelaani vikali shambulio la Israel dhidi ya Hospitali ya al Ahli-Arab iliyopo kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Hospitali hiyo ilikuwa inafanya kazi ikiwa na wagonjwa, wafanyakazi wa afya na watu waliolazimika kuhama makazi yao na kujipatia hifadhi Hospitalini hapo. Ripoti za awali zinaonyesha shambulio hilo limesababisha mamia ya vifo na majeruhi.

Hospitali hiyo ilikuwa moja kati ya hospitali 20 kaskazini mwa Ukanda wa Gaza zilizopewa amri ya kuondoka na jeshi la Israel. Amri hiyo ya kuondoka imekuwa ngumu kutekelezwa kutokana na hali ya kutokuwa na usalama, hali mbaya ya kuwepo kwa wagonjwa wengi, ukosefu wa magari ya wagonjwa, wafanyakazi na Hospitali hiyo kutumika kama makazi mbadala kwa wale waliohamishwa, imesema WHO  katika taarifa yake.

WHO imetoa wito wa raia pamoja na vituo vya Afya kulindwa.

"Amri za kuondoka lazima zifutiliwe mbali. Sheria ya kimataifa ya Haki za Binadamu lazima iheshimiwe, sheria inasema huduma za afya ni haki na hivyo lazima zilindwe kwa dhati na kamwe zisishambuliwe," imesema WHO.

 


Post a Comment

0 Comments